Home » » MA DC WAASWA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATAJI MITI OVYO

MA DC WAASWA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATAJI MITI OVYO


 
Na Hastin Liumba, Sikonge-Tabora yetu
 
SERIKALI imeagiza Wakuu wa wilaya kulinda ipasavyo misitu iliyopo
katika maeneo yenye yao ili kuhifadhi maliasili zote zilizopo katika
wilaya hizo ikiwemo vyanzo vya maji.
 
Agizo hilo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Tabora Suleiman Kumchaya kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Fatma Mwassa wakati akifungua mkutano wa
ujirani mwema uliofanyika katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora
ukijumuisha Ma DC, Wakurugenzi, Ma DAS, wakuu wa idara na wajumbe wa
kamati ya ulinzi na usalama.
 
Akizungumza na wajumbe hao toka wilaya za Mbozi, Mbalali, Momba,
Nkasi, Mpanda, manyoni, kalambo, Chunya, Mlele, Sumbawanga, Rukwa,
Kasulu, Uvinza na mwenyeji Sikonge, amesema tatizo kubwa
linalozikabili wilaya hizo ni vitendo vya ukataji miti ovyo
vinavyozidi kuongezeka siku hadi siku na hivyo kukaribisha jangwa
katika maeneo hayo.
 
‘Nawaombeni sana waheshimiwa wakuu wa wilaya kuweni makini katika hili
na mchukue hatua vinginevyo hali ya jangwa inanukia katika wilaya
zenu’, alisema.
 
Amewataka kujadili kwa kina tatizo hilo ili watoke na kauli moja
itakayoweza kulinda au kuamua mstakabali wa kuendelea kustawi misitu
hiyo ya asili na maliasili zote zilizomo.
 
Aidha amewataka kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano katika ukanda huo
unaounganisha mikoa ya Katavi, Rukwa, Mbeya, Singida, Kigoma na Tabora
ili kurahisisha upashanaji taarifa sambamba na kubadilishana uzoefu wa
kiutendaji katika kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kwa kiasi
kikubwa uharibifu wa mazingira.
 
Pia amewataka kuhamasisha suala la ulinzi shirikishi katika maeneo yao
sambamba na kuweka mikakati thabiti itakayosaidia kuimarisha utunzaji
wa misitu ya asili, vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
 
Ma DC hao pia wametakiwa kuwa makini na ufugaji wa kuhamahama kwani
umekuwa ukichangia kwa kiwango kikubwa uharibifu wa mazingira, hivyo
akawataka watoke na kauli moja iliyothabiti juu ya uharibifu huo wa
mazingira na vyanzo vya maji.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa