Home » » WASUKUMA WAASWA KUACHANA NA UTAMADUNI WA ‘CHAGULAGA’

WASUKUMA WAASWA KUACHANA NA UTAMADUNI WA ‘CHAGULAGA’


 
Na Hastin Liumba, Sikonge- Tabora yetu Blog 
JAMII ya wasukuma imeaswa kuachana na mila ya CHAGULAGA kwa kuwa
inahatarisha maisha ya vijana hususani wa kike kwa kuchochea ngono zembe na
pia kuwakosesha fursa ya kwenda shule.
 
Rai hiyo imetolewa juzi na Afisa Utamaduni wilaya ya Sikonge mkoani Tabora
Xavery Malapwa,  katika mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti hili.
 
Amesema mila hiyo ya kisukuma inayomaanisha ‘chagua unayemtaka’ inapendwa
sana na jamii hiyo lakini ni ukweli usiofichika kwamba inamnyima mtoto wa
kike uhuru wa kuchagua mwanaume anayempenda kwa vile hulazimishwa kuchagua.
 
‘Hii mila imepitwa na wakati kwa kuwa inamlazimisha msichana kuchagua
mwanaume katika kundi kubwa la wanaume hata kama hakuna anayempenda kwa
dhati kati yao’, alisema.
 
 Alisema Wasukuma wanaitumia kama njia ya kudumisha utamaduni wao wa jadi
lakini utamaduni huo umeanza kuingiliwa na utandawazi wa kimapenzi na sio
mila tena.
 
Ameongeza kuwa kitendo cha wazazi kuhamasisha mabinti zao kwenda katika
mikusanyiko ya ngoma, minada au magulio ili kukutana na wanaume ni
unyanyasaji, sio ustaarabu na hakifai kwa sababu kinawanyima uhuru wa
kuamua, kibaya zaidi katika maeneo hayo mapenzi yako nje nje na hawatumii
kinga.
 
Anafafanua kuwa mabinti wanapoenda katika minada au ngoma mara nyingine
hujikuta wamezungukwa na kundi kubwa la vijana wa kiume na kila mmoja
huchagua anayemtaka hali ambayo wakati mwingine husababisha ugomvi baina
yao.
 
‘Nashauri utamaduni huo uachwe, wazazi katika jamii hiyo waelimishwe
madhara yanayoambatana na kuendelea kudumisha mila hiyo, hasa maambukizi ya
VVU, badala yake waanze kuwahamasisha mabinti zao kwenda shule na sio
kuozeshwa’, alisema.
 
Malapwa aliungana na baadhi ya viongozi wa vijiji katika wilaya ya Sikonge
kuiomba serikali kuingilia kati suala hilo huku akibainisha umuhimu wa
wazazi hao kupewa elimu sahihi ya malezi bora kwa watoto wa kike hasa wale
walioko katika maeneo ambayo mila hiyo inaendelea kudumishwa ili kuwaepusha
na maambukizi ya VVU.
 
Aliongeza kuwa ni vigumu kwa wazazi hao kuacha mila hiyo mara moja kwa
sababu ya mazoea,   ila kinachotakiwa ni kuendelea  kuwaelimisha umuhimu wa
kuacha mila hiyo na kupeleka watoto wao shule hususani wa kike.
 
Malapwa alitoa wito kwa jamii nzima kushirikiana na viongozi wa vitongoji,
vijiji, kata na wilaya kuwaelimisha na kuwahimiza wazazi hao kuachana na
mila hiyo kwani ikiendelea namna hiyo madhara yake ni makubwa hususani
maambukizi ya VVU na kuongeza vitendo vya uhasama na chuki baina ya vijana
hao.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa