Home » » WILAYA 17 WATOA TAMKO LA PAMOJA KUMPONGEZA JK

WILAYA 17 WATOA TAMKO LA PAMOJA KUMPONGEZA JK


 
Na Hastin Liumba, Sikonge
 
WILAYA 17 hapa nchini wametoa tamko rasmi la kumpongezi Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwa jitihada
zake za dhati za kuanzisha ‘Oparesheni Kimbunga’ na ‘Oparesheni
tokomeza Ujangili’ ili kulinda usalama wa raia na rasirimali za nchi.
 
Tamko hilo limetolewa na Wakuu wa wilaya zipatazo 17 katika mkutano wa
ujirani mwema uliofanyika wilayani Sikonge mkoani Tabora  ambao
uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 200 kutoka mikoa ya Katavi, Mbeya,
Singida, Rukwa, Kigoma na Tabora.
 
Walisema oparesheni hiyo imekuwa na manufaa makubwa sana katika maeneo
mengi hapa nchini kwani imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa
vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vikifanywa na wahamiaji haramu
sambamba na kukamatwa kwa silaha lukuki zilizokuwa zimefichwa katika
maeneo mbalimbali.
 
Wakuu hao wamebainisha kuwa agizo la Rais Kikwete la kuanzisha kwa
oparesheni hiyo lilikuwa sahihi na lilikuja kwa wakati mwafaka kwani
uharibifu, mauaji, utekaji magari, uwindaji holela wa tembo na wizi wa
nyara za serikali vilikuwa vimekithiri kiasi cha kuhatarisha amani na
rasilimali za taifa.
 
‘Kwa kauli moja tunaunga mkono oparesheni hiyo na tunaomba oparesheni
hizo ziendelee kwa faida ya wananchi wetu kwa kuwa zinatusaidia sana
kurahisisha utekelezaji wa majukumu yetu ya kusimamia usalama wa raia
na rasilimali zote zilizopo katika hifadhi zetu’. walisema.
 
Wakuu hao pia walitoa tamko rasmi la kufungwa kwa shughuli zote za
uvuvi katika ziwa Rukwa kutokana na kukumbwa na upungufu mkubwa wa
samaki wadogo na wakubwa uliotokana na uvuvi haramu ambao umechangia
kwa kiasi kikubwa kumalizika kwa samaki wakubwa katika ziwa hilo.
 
‘Kwa sababu samaki wamepungua  sana katika ziwa Rukwa, tumekubaliana
kulifunga kwa kipindi cha miezi 6 kuanzia mwezi Januari mosi 2014 ili
samaki waongezeke na wananchi watatangaziwa uamuzi huu kabla ya mwezi
Desemba 15 2013’. alisema Mwenyekiti wa mkutano huo Deodatus Kinawiro,
DC wa Chunya.
 
Wamefafanua uamuzi wa kulifunga ziwa hilo umepata baraka zote toka
wizara husika na wakazi wanaoishi jirani na ziwa hilo hususani wilaya
za Chunya, Mlele, Sumbawanga na zinginezo wameshataarifiwa kufungwa
kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo kuanzia mwezi Januari.
 
Mkutano huo umehudhuriwa na wakuu wa wilaya, makatibu tawala,
Wakurugenzi, Maafisa usalama, wakuu wa polisi wilaya, wajumbe wa
kamati za ulinzi na usalama.
 
Wengine ni wakuu wa idara kutoka wilaya za Mbarali, Mbeya, Momba,
Nkasi, Mpanda, Manyoni, Kalambo, Chunya, Mlele, Sumbawanga, Sikonge,
Urambo, Kaliua, Kasulu na Uvinza.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa