MADIWANI katika halmashauri
ya wilaya ya Sikonge wametaka kukamilishwa ujenzi wa vituo vya Afya
unaosuasua katika baadhi ya Kata.
Hayo yamebainishwa
katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo
kilichoketi kwa ajili ya kupitisha bajeti ya maendeleo kwa kipindi cha
mwaka wa fedha 2014/2015.
Diwani wa kata ya
Tutuo, Mh.Rashid Magope amesema anasikitishwa na ujenzi wa kituo cha Afya Tutuo
kutokamilika wakati fedha ilishatengwa na akaomba halmashauri ikamilishe
haraka ujenzi wake kwani wananchi wake wanahangaika sana kutafuta huduma za
Afya.
Naye diwani wa kata
ya Kipili, Mh.Hamid Manzi ameomba halmashauri hiyo ifanye kila iwezalo ili
ujenzi wa kituo cha afya Kipili ukamilike haraka kwa kuwa kituo hicho ni
mkombozi pekee kwa wananchi wake kwani wanalazimika kutembea umbali mrefu sana
kutafuta huduma za afya.
Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri hiyo Shadrack Mhagama akifafanua hoja za madiwani hao amesema
halmashauri yake imetenga fedha za kutosha kushughulikia mapungufu mbalimbali
yanayovikabili vituo vya afya ikiwemo hospitali ya Mazinge na kituo cha afya
Tutuo.
Amesema kero
zinazokikabili kituo cha afya Kipili zinafahamika hivyo akabainisha kuwa
wamejipanga kuzifanyia kazi katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao 2015/2016 kwa
sababu kero za namna hiyo ni nyingi hawawezi kuzitatua zote kwa bajeti ya mwaka
huu wa fedha.
Aidha amebainisha
kuwa katika bajeti ya mwaka 2014/2015 wameweka kipaumbele cha kutatua
kero katika hospitali ya Mazinge,zahanati ya Mwenge iliyoko katika kata ya
Kitunda na Mwamayunga iliyoko katika kata ya Kisanga.
0 comments:
Post a Comment