Na Hastin Liumba, Tabora
MKURUGENZI Mtendaji wa Manispaa ya Alfred Luanda ameazimia kuboresha
hali ya usafi wa mazingira ili kumaliza kero ya uchafu katika mji huo.
Hayo aliyasema wakati akiongea na gazeti hili ofisini kwake uhusiana
na hali ya usafi katika manispaa ya Tabora kwa kipindi hiki cha mvua
za masika.
Luanda alisema ipo haja sasa wananchi kwa kushirikiana na watendaji wa
manispaa kuweka mazingira kwenye hali ya usafi hasa kipindi hiki cha
mvua kwani kunaweza kutokea magonjwa ya milipuko.
Alisema hali ya usafi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo
imekuwa si ya kuridhisha kwa muda mrefu hasa katika vyoo vya umma,
masoko na mitaa lakini jitihada zinzfanyika kumaliza kero hiyo.
Aliongeza kuwa suala la usafi na mikakati ya kuboresha mazingira kwa
ujumla katika mji wa Tabora limekuwa likijadiliwa katika vikao
mbalimbali lakini utekelezaji wake umekuwa unasuasua kwa madai ya
ukosefu wa fedha za kufanikisha mpango huo.
‘Ndugu yangu hili la uchafu sio la kufumbia macho hata kidogo, ndio
maana nimeandaa mkakati maalumu wa kubadilisha hali hii, nimewaomba
madiwani na watendaji wote tushirikiane kwa pamoja ili mazingira yetu
yaanze kupendeza’, alisema.
Alisema ili kufanikisha mpango huo yatanunuliwa makontena mapya 30
ambayo yanagharimu kiasi cha sh milioni 300, kukarabati magari ya
kubebea taka kwa gharama ya sh milioni 10, kununua vikapu 50 vya
kutupa taka katika mitaa mbalimbali kwa sh milioni 1.5 na kuweka
utaratibu wa faini kwa wanachi watakaoendelea kuchafua mazingira kwa
makusudi.
Nao madiwani kadhaa walisema wanashukuru Mkurugenzi huyo kwa kuanza
kubadilisha mandhari ya mji wetu, kinachotakiwa sasa ni kumpa
ushirikiano wa dhati ili kufanikisha mpango huo.
Walisema hatua yake ya sasa katika kufanya matengenezo ya magari
mabovu ya kuzoa taka, ununuzi wa mapipa ya uchafu na mengineyo, ni
ishara njema ya kuelekea usafi wa mji wetu.
Home »
» MKURUGENZI MANISPAA KUSIMAMIA USAFI.
0 comments:
Post a Comment