Home » » Mwekezaji vitalu vya uwindaji apigwa ‘stop’

Mwekezaji vitalu vya uwindaji apigwa ‘stop’

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, limewakataa mwekezaji, Shen na wenzake Wembele Hunting Safaris wanaofanya kazi za uwindaji katika pori la misitu ya hifadhi iliyoko wilayani humo.
Tamko hilo limetolewa katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kilichoketi  juzi katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, FDC, wilayani humo.
Akitoa taarifa ya uamuzi huo kwa niaba ya madiwani, watendaji wa halmashauri na wananchi, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Robert Kamoga, alisema wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji, ubabe, dhuluma, wizi na uonevu unaofanywa na wawindaji walioko katika mapori ya hifadhi wilayani humo.
Alisema wawekezaji hao wanajifanya miungu watu na hawajui kama mapori hayo  ni mali ya serikali na msimamizi wake mkuu ni serikali ya wilaya kupitia baraza la madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo.
Alisema mwekezaji Shen kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa kero kwa wananchi wanaoishi karibu na misitu hiyo na anadaiwa kujimilikisha kwa nguvu hifadhi za misitu ya Tulu, Koga, Kululu na Inyonga East wilayani humo huku akiuza wanyama na vitalu vya uwindaji kwa wenzake.
“Hawa watu wakati wanaingia walipokewa vizuri  na kupewa ushirikiano na JUHIWAI (Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyama Pori Ipole), lakini sasa wanataka kujifanya wao ndio serikali, wanauza vitalu vya uwindaji, wanapiga wananchi ovyo, wanadharau viongozi wa halmashauri akiwemo Mbunge wa Sikonge, ni lazima waondoke,” alieleza
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa