BARAZA la Madiwani katika
halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limemkataa mwekezaji
anayejishughulisha na uwindaji katika pori la misitu ya hifadhi iliyoko
wilayani humo kwa vitendo vya unyanyasaji wananchi, kuuza wanyama na vitalu vya
uwindaji kiholela.
Akitoa taarifa ya
uamuzi huo kwa niaba yaMadiwani, watendaji wa halmashauri na wananchi wote wa
wilaya hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Robert Kamoga amesema wamechoshwa
na vitendo vya unyanyasaji, ubabe, dhuruma, wizi na uonevu unaofanywa na
wawindaji walioko katika mapori ya hifadhi wilayani humo.
Amesema wawekezaji
hao wanajifanya miungu watu na hawajui kama mapori hayo ni mali ya
Serikali na msimamizi wake mkuu ni Serikali ya wilaya kupitia Baraza la
madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo, kibaya zaidi hawatambui kuwa wako
chini ya mamlaka ya serikali.
Mwekezaji huyo
anayejulikana kwa jina la SHEN kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa kero kwa
wananchi wanaoishi karibu na misitu hiyo ya hifadhi na anadaiwa kujimilikisha
kwa nguvu hifadhi za misitu na Koga.
Aidha mwekezaji huyo
anadaiwa kuuza raslimali zilizoko katika hifadhi hizo huku akidai kuwa ana
Ramani toka wizarani inayomruhusu kumiliki eneo lote la tarafa ya Kiwere na
kufanya chochote anachotaka ndio maana anatoa vitisho vya kuwahamisha kwa nguvu
wananchi wote wanaoishi karibu na misitu hiyo wilayani humo.
Mwenyekiti wa CCM
wilayani Sikonge ,Bw.Abisai Mbogo amepongeza uamuzi huo wa Madiwani na kuongeza
kuwa hakuna Serikali inayoweza kuruhusu mikataba ya namna hiyo ya kumiliki
hifadhi za misitu ya Serikali katika wilaya nzima na kibali cha kunyanyasa
wananchi, hiyo mikataba ni feki ipitiwe upya, tenda zitangazwe upya na uamuzi
wa kuwafukuza ni halali kabisa.
0 comments:
Post a Comment