WANANCHI wa kitongoji cha Mwayunge mjini Igunga mkoani Tabora
wameulalamikia uongozi wa wilaya hiyo kwa kushindwa kudhibiti maafa
yanayotokea kila mwaka nyakati za masika.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wananchi hao
walisema kuwa maafa hayo yamekuwa yakitokea kila mwaka katika
kitongoji chao kutokana na maji kujaa na kukosa mwelekeo.
Wananchi hao walisema kuwa dimbwi lililopo katika kitongoji hicho
hujaa maji wakati wa mvua za masika zinapoanza kunyesha na kuingia
katika nyumba za watu na kusababisha maafa hayo.
Walisema kuwa ni zaidi ya miaka mitatu maafa hayo yameendelea
kujitokeza na kusababisha athari kwa wananchi baada ya nyumba zao
kuharibiwa na mvua hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Selemani Saidi, alisema kuwa
halmashauri ya wilaya hiyo inatumia gharama kubwa pindi yanapotokea
maafa huku wakisahau kuchimba mitaro ili maji hayo yapate mwelekeo na
kuepusha maafa hayo.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji, Ally Isike, alisema kuwa halmashauri ya
wilaya hiyo imeahidi kuchimba mitaro ya kupitisha maji hayo, lakini
hadi sasa bado haijatekelezwa.
Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo,
Rustika Turuka alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la maafa kila mwaka na
kusema kuwa amejipanga kutatua kero hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment