WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu katika machimbo madogo ya Mwanshina
katika Kijiji cha Nhobola wilayani Nzega mkoani Tabora, wameiomba
serikali kuwapatia kibali cha kuchimba dhahabu pembezoni mwa mgodi
mkubwa wa Resolute ili wakidhi mahitaji yao.
Wakizungumza katika mkutano wa kijiji mbele ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya
Nzega, Bituni Msangi, walisema kuwa serikali kupitia Waziri wa Nishati
na Madini, Prof. Sospeter Muhongo awape kibali cha kuendesha shughuli
zao kutokana na mwekezaji wa mgodi huo kukamilisha shughuli za
uchimbaji mwaka 2015.
Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Joseph Mabondo alisema kuwa mgogoro
uliopo kati yao na serikali ni kutokana na kukosa eneo la kuchimba
dhahabu huku wawekezaji wakiwa na eneo kubwa wasilotumia.
Joseph aliiomba serikali kusikiliza kilio hicho ili waweze kupatiwa
kibali cha kuchimba dhahabu kwa uhuru kama ilivyo katika baadhi ya
sehemu nyingine.
Alisema kuwa kitendo cha kuwapiga marufuku na kuwafukuza katika
machimbo hayo kinajenga mahusiano mabaya kati yao na serikali wakati
wana haki ya kupewa nafasi ya kuchimba ili kukidhi mahitaji yao na
kukuza uchumi.
“Tunamuomba waziri husika na naibu wake Maselle watusaidie suala hili
ili tuweze kujikwamua kimaisha kwani mambo ya kukimbizana na
kufukuzana sio mazuri, inapaswa kutuangalia kwa macho mawili ili nasi
tunufaike na rasilimali zetu,’’ alisema.
Alisema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki maeneo
makubwa na kuyatumia katika shughuli zao za uchimbaji wakati wachimbaji
wadogo nao wanaweza kuyaendeleza kwa haraka zaidi.
Naye DC Msangi alisema kuwa amesikia kilio cha wachimbaji hao na
kuahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi
na usalama ya wilaya hiyo ili kumshawishi mwekezaji wa mgodi huo
kuwapatia eneo hilo
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment