Home » » MWEKEZAJI WA VITALU VYA UWINDAJI APIGWA ‘STOP

MWEKEZAJI WA VITALU VYA UWINDAJI APIGWA ‘STOP

Na Hastin Liumba, Sikonge
 
BARAZA la madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora
limewakataa mwekezaji aitwaye SHEN na wenzake Wembele Hunting Safaris
za wanaofanya kazi za uwindaji katika pori la misitu ya hifadhi
iliyoko wilayani humo.
 
Tamko hilo limetolewa katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa
halmashauri ya wilaya hiyo kilichoketi  juzi katika ukumbi wa Chuo cha
Maendeleo ya wananchi, FDC, wilayani humo.
 
 
Akitoa taarifa ya uamuzi huo kwa niaba ya madiwani, watendaji wa
halmashauri na wananchi wote wa wilaya hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo Robert Kamoga amesema wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji,
ubabe, dhuruma, wizi na uonevu unaofanywa na wawindaji walioko katika
mapori ya hifadhi wilayani humo.
 
Amesema wawekezaji hao wanajifanya miungu watu na hawajui kama mapori
hayo  ni mali ya serikali na msimamizi wake mkuu ni serikali ya wilaya
kupitia baraza la madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo, kibaya
zaidi hawatambui kuwa wako chini ya mamlaka ya serikali.
 
Mwekezaji huyo  SHEN kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa kero kwa
wananchi wanaoishi karibu na misitu hiyo ya hifadhi na anadaiwa
kujimilikisha kwa nguvu hifadhi za misitu ya Tulu, Koga, Kululu na
Inyonga East wilayani humo huku akiuza wanyama na vitalu vya uwindaji
kwa wenzake.
 
‘Hawa watu wakati wanaingia walipokelewa vizuri  na kupewa ushirikiano na
JUHIWAI (Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyama Pori Ipole), lakini sasa wanataka
kujifanya wao ndio serikali, wanauza vitalu vya uwindaji, wanapiga wananchi
ovyo, wanadharau viongozi wa halmashauri akiwemo mbunge wa Sikonge, ni
lazima waondoke,’ alisongeza.
 
Mwekezaji huyo inadaiwa kuwa anashirikiana na kampuni ya Wembele
Hunting Safaris inayofanya shughuli za uwindaji katika pori la wazi la
hifadhi
linalozunguka vijiji vyote vya kata ya Kitunda katika tarafa ya Kiwere
ikipakana na hifadhi ya Rungwa iliyoko wilayani Manyoni na hifadhi ya
Katavi, na wote wanadaiwa kuingia kinyemela.
 
‘Huyo SHEN na wenzake wote hatuwataki katika misitu yetu, tunataka serikali
itangaze upya zabuni hiyo ya uwindaji, waondoke mara moja,
wasipoondoka  wananchi watawaondoa kwa maandamano makubwa, kwa sasa
hivi tunafuatilia mikataba yao tu’, walikazia madiwani hao.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa