Home »
» WAKULIMAWA TUMBAKU ATENGA MIL.5.1/- ZA UMEME
WAKULIMAWA TUMBAKU ATENGA MIL.5.1/- ZA UMEME
CHAMA
cha Msingi cha Wakulima wa Tumbaku katika Kata ya Kisanga wilayani
Sikonge mkoani Tabora kimetenga sh. milioni 5.1 za mauzo ya tumbaku kwa
msimu wa 2013/2014 kwa ajili ya kutunisha mfuko maalumu wa kuweka umeme
katika kata hiyo yenye vijiji 3.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa
chama hicho, Rashid Mazinge, katika taarifa yake kwa waandishi wa
habari waliotembelea kijiji hicho wiki iliyopita. Alisema chama hicho
chenye wanachama 700 kimekusudia kuweka umeme katika makao makuu ya kata
hiyo yaliyoko katika kijiji cha Kisanga na vijiji vyake na kwa kuanzia
wameanzisha mfuko maalumu wa umeme kwa ajili ya kutimiza lengo hilo.
Alisema
wametenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya maandalizi ya awali ambapo
wataanza kwa kununua vifaa mbalimbali vya umeme ikiwemo vifaa vya
kompyuta na printa vitakavyosaidia kurahisisha shughuli mbalimbali za
kiofisi katika ofisi ya chama hicho, tayari kompyuta kadhaa
zimeshanunuliwa.
"Ndugu waandishi wa habari, tumekusudia kuweka
umeme katika kijiji chetu ndiyo maana tumeanza kukusanya fedha na
kuzitunza kama wanakikundi, muda si mrefu tutaenda wilayani kufuatilia
taratibu zingine, tunaomba na ninyi mtusaidie huko wilayani ili
tufanikiwe haraka", alisema.
Alibainisha kuwa chama kimefikia hatua
hiyo baada ya kupata mafanikio makubwa katika msimu wa 2012/2013 na
2013/2014 hali iliyowafanya wanachama wake kwa kauli moja kuridhia haja
ya kuanzishwa mfuko huo ili kujiletea maendeleo katika kata hiyo yenye
vijiji 3 (Utyatya, Mwamayunga na Kisanga).
Katika msimu wa 2012/2013
chama hicho kilizalisha jumla ya kilo 940,049 za tumbaku zenye thamani
ya dola za Marekani 2,538,132 (sawa na sh. bilioni 4.1) na mapato ya
ushuru yalikuwa dola za Marekani 65,000 (sawa na sh. milioni 103.4), kwa
mapato hayo waliweza kulipa deni la pembejeo la dola 692,000.(sawa na
sh. bilioni 1.1) kutoka benki ya NMB na kubakiwa na fedha ya kutosha.
Aidha
katika msimu wa 2013/2014 walilenga kuzalisha jumla ya kilo 1,400,000
zenye thamani ya dola 3,920,000 sawa na sh bilioni 6.3 na mapato ya
ushuru walilenga kukusanya dola 98,000 sawa na sh. milioni 156.8 hali
ambayo itawawezesha kulipa deni la pembejeo dola 968,000 sawa na sh.
bilioni 1.5 toka NMB.
Alitaja mafanikio ya chama hicho kuwa ni
kuanzishwa mfuko wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia tumbaku ambao
umetengewa kiasi cha dola 31,000 (sh milioni 49.3), ujenzi wa ofisi ya
kata ambapo chama hicho kimechangia sh. milioni 3, kuanzisha mfuko wa
umeme, kuanzisha KISANGA SACCOS LTD ambayo mpaka sasa ina jumla ya dola
21,000 (sawa na sh. milioni 33,495,000).
Alisema chama hicho
kimedhamiria kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo kupitia vikao
mbalimbali vya wanachama wake ambapo kimetenga sh milioni 30 kwa ajili
ya ununuzi wa gari aina ya FUSO ili kurahisisha huduma mbalimbali za
wakulima kijijini hapo, pia kimekusudia kukusanya dola 84,000 (sh.
milioni 134,000,000) ili kuongeza nguvu ya SACCOS yao.
Pamoja na
mafanikio hayo zipo changamoto kadhaa zinazowakabili ikiwemo mikopo na
bei kubwa za pembejeo, ucheleweshaji na upatikanaji wa pembejeo hizo,
kutokuwa na umeme, ubovu wa barabara zinazounganisha vijiji hivyo,
ukosefu wa maji safi na salama, ukosefu wa nyumba ya mganga wa zahanati
na kituo cha polisi.
Diwani wa kata hiyo Abdallah Msumeno mbali na
kupongeza hatua ya chama hicho kutenga sh. milioni 2 kwa ajili ya
kununua viti 100 vya plastiki na kutenga sh 576,000 za michango ya
wanachama katika mfuko wa NSSF pia ametoa wito kwa wakulima hao kufuata
kalenda ya msimu wa kilimo ili kupata mafanikio zaidi.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment