Home »
» WILAYA YA SIKONGE YAPONGEZWA
WILAYA YA SIKONGE YAPONGEZWA
HALMASHAURI
ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora imemwagiwa pongezi kwa jitihada zake
za dhati na uthubutu wa kuwainua vijana kwa kuwaanzishia kituo maalumu
cha ujasiriamali kitakachowapa ujuzi wa aina mbalimbali.
Pongezi
hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa na wajumbe
mbalimbali wa kamati ya ushauri ya mkoa katika kikao kilichofanyika wiki
iliyopita mjini hapa.
Mwassa alimwaga pongezi hizo baada ya
kufurahishwa na uanzishwaji wa kituo hicho cha vijana wilayani humo
ambacho mpaka sasa kina vijana wakike na wakiume wasiopungua 100.
Alisema
halmashauri ya wilaya hiyo ni mfano wa kuigwa katika mkoa huo na
inastahili kupongezwa kwa kitendo chao cha kuthubutu kuanzisha kituo
pasipo kuangalia changamoto zozote zilizoko mbele yao hususani gharama
za kuwaweka vijana wote hao mahali pamoja kwa mwaka mzima.
"Ndugu
wajumbe naomba niseme hili, Sikonge imetupaisha, ni halmashauri pekee
hapa nchini iliyoonesha uthubutu wa kiwango cha juu katika kuhakikisha
vijana wa kike na kiume wanawekewa utaratibu maalumu wa kuwainua
kiuchumi, kwa kweli wamefanikiwa, naomba kila halmashauri iige mfano
huo," alisema.
Alisema vijana hao tayari wameshaanza kupewa ujuzi wa
aina mbalimbali wa stadi za maisha kupitia nadharia na vitendo katika
maeneo ya ufugaji kuku, mbuzi na ng'ombe, kilimo cha kisasa cha mazao
mbalimbali, utengenezaji mizinga na ufugaji nyuki wa kisasa.
Ujuzi
mwingine unaotolewa na wataalamu mbalimbali kwa vijana hao ni ufyatuaji
matofali kwa njia za kisasa, ufundi seremala, uashi na fani nyinginezo.
Aliwapongeza
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rober Kamoga, DC Hanifa Selengu,
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Shadrack Mhagama, Mbunge Said Nkumba na
Watendaji wote kwa jitihada zao za kuhakikisha vijana hao zaidi ya 100
wanapata mwanga mpya wa kimaisha ili wakawe walimu wazuri kwa vijana
wenzao.
Kituo hicho kilichopewa jina la 'Pathfinder Green City'
kimeshatembelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Balozi Hamis
Kagasheki na mawaziri wengine na wote walimwaga pongezi nyingi kwa
uongozi wa wilaya hiyo sambamba na kuahidi misaada lukuki.
Aidha
Mwassa aliagiza kila halmashauri katika mkoa huo itenge bajeti maalumu
kwa ajili ya kuanzisha au kusaidia miradi mbalimbali ya vijana na katika
mwaka wa fedha 2014/2015 kila halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya
shughuli hiyo kama ifuatavyo Sikonge sh. milioni 365, Kaliua sh. milioni
100, Uyui sh. milioni 240, Urambo sh. milioni 290, Nzega sh. milioni
150, Tabora sh. milioni 180 na Igunga sh. milioni 200
Chanzo;MAJIRA
0 comments:
Post a Comment