Na Hastin Liumba, Sikonge
ASASI ya Uhai Mazingira (UMA) yenye makao yake makuu wilayani Sikonge
mkoani Tabora imeanzisha operesheni maalumu itakayosaidia kuokoa
uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi mtendaji wa asasi hiyo Athega Ismail
katika hafla fupi ya uzinduzi wa mafunzo ya utunzaji mazingira na
uhifadhi wa vyanzo vya maji yaliyoambatana na zoezi la upandaji miti
katika kijiji cha Pangale wilayani Sikonge.
Alisema mradi huo ambao utatekelezwa katika vijiji vyote vya kata za
Pangale, Tutuo na Chabutwa wilayani Sikonge umelenga kutoa mafunzo kwa
wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, uhifadhi wa vyanzo vya
maji na upandaji miti kwa kila kaya.
Alisema wameamua kujikita katika shughuli ya utunzaji mazingira na
uhifadhi wa vyanzo vya maji baada ya kushuhudia vitendo vya uharibifu
wa mazingira vikizidi kuongezeka siku hadi jambo ambalo athari zake ni
kubwa sana kwa viumbe hai.
'Ndugu zangu maeneo mengi hapa nchini ikiwemo wilaya yetu ya Sikonge
yameathiriwa na uharibifu wa mazingira hali ambayo imechangia kupotea
kwa uoto wa asili na maeneo hayo kubaki jangwa' alisema.
Aidha aliongeza vitendo vya ukataji miti ovyo na uchomaji mkaa
vinavyofanywa na wakulima katika maeneo mengi wilayani humo vimeathiri
kwa kiwango kikubwa ustawi wa mazingira katika wilaya hiyo na hivyo
kuharibu uoto wa asili na vyanzo vya maji.
Alisema uzoefu unaonyesha katika maeneo yaliyo mengi mwitikio wa
wananchi katika utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji
ni mdogo sana hali inayosababishwa na elimu duni.
Alisema ili kufanikisha zoezi hilo Ismail aliomba wananchi wajitokeze
kwa wingi katika mafunzo watakayoendesha katika kata hizo ili
utekelezaji wa mradi huo uweze kuwa na tija katika maeneo hayo kwa
faida ya vizazi vyao.
Katika uzinduzi wa shughuli za asasi hiyo ulioongozwa na Mkuu wa
wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu, miti zaidi ya 100 ilipandwa katika
kata ya Pangale huku lengo likiwa kupanda miti 5000 katika kata hizo
tatu.
Home »
» UMA' YAZINDUA OPERESHENI OKOA MAZINGIRA SIKONGE
UMA' YAZINDUA OPERESHENI OKOA MAZINGIRA SIKONGE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment