Home » » MAJI YAWAGAWA MADIWANI IGUNGA

MAJI YAWAGAWA MADIWANI IGUNGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399

MRADI mkubwa wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria, umeligawa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kutokana na bomba kupitia kwenye vijiji vyenye maji na kuacha ambavyo vina uhaba.
Mradi huo unaotarajiwa kupunguza kero ya maji kwa Wilaya za Nzega, Igunga na Tabora Mjini, unatarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni kwa ufadhili wa serikali ya India.
Wakizungumza katika kikao hicho, baadhi ya madiwani walisema mradi huo umepitia vijiji ambavyo havina shida ya maji huku vyenye shida kubwa vikiachwa bila kupatiwa mradi.
Diwani wa Kata ya Isakamaliwa, Dotto Kwilasa, alisema mradi huo umeligawa jimbo la Igunga kutokana na sehemu kubwa ya wananchi wenye shida ya maji kukosa mradi huo huku vijiji ambavyo havina shida vikiendelea kupitiwa na mradi huo.
“Kanda ya Kaskazini tumetengwa jamani, kila mradi unakwenda Kusini tu, viongozi wakubwa wa kitaifa na wale wa chama wakija wanaulizwa na wananchi juu ya maji na wao wanadai maji mtayapata ya Ziwa Victoria…leo bomba la maji mnalipitisha kwenye vijiji vyenye maji, tutawaambiaje wananchi?” alisema Dotto.
Naye Diwani wa Nsungwizi, Athumani Henry, alisema makosa hayo yametokana na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kupendekeza vijiji bila kushirikisha kamati husika ambayo ingeweza kutoa mapendekezo ili wananchi ambao wana shida ya maji wapate
huduma hiyo.
Alisema kitendo hicho kilichofanywa na watendaji, hakifai kurudiwa tena kutokana na wananchi wengi kukosa fursa ya kupata mahitaji stahiki ya maji na kuongeza uhasama kati ya serikali na wananchi.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Igunga, Raphael Melumba, alisema kazi ya kutafuta eneo bomba hilo la maji lipitie ilifanywa na wapembuzi wa mradi huo na kwamba hakuna kiongozi wa Wilaya aliyeshirikishwa juu ya vijiji utakapopitia mradi huo.
Melumbe, alisema vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo, utasambazwa kwa vijiji jirani kwa kilometa 12 kutoka kijiji husika na kuongeza, jitihada mbalimbali za halmashauri zitafanyika ili kuyavuta maji hayo katika vijiji husika.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Abubakar Shaaban, aliwataka madiwani hao kushukuru kupata mradi huo kutokana na baadhi ya Wilaya kukosa kabisa mradi huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, alisema mradi huo ni wa serikali kuu, hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kubadili njia ya maji hayo na kuwataka madiwani hao kuwa wavumilivu, ikiwa na kupanga mipango ya kuyasogeza maji hayo katika vijiji ambavyo havitafikiwa
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa