Home » » RAS TABORA AWAFUNDA WASHIRIKI WA MAFUNZO KUHUSU MWONGOZO WA USIMAMIZI WA UWEKEZAJI WA UMMA

RAS TABORA AWAFUNDA WASHIRIKI WA MAFUNZO KUHUSU MWONGOZO WA USIMAMIZI WA UWEKEZAJI WA UMMA

Dkt. Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango, akitoa neno kwa Maofisa na watendaji wa Idara za Sera na Mipango kutoka mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Katavi ambao ni washiriki wa mafunzo yanayohusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kabla ya kumkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara  (wa pili kushoto) Wengine ni Dkt. Jehovaness Aikaeli, Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Bibi Rukia S. Manduta, Katibu Tawala Msaidizi, Mipango na Uratibu Mkoa wa Tabora.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara  (aliyesimama) akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kwa Maofisa na watendaji wa Idara za Sera na Mipango kutoka mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Katavi. Wengine ni Bi. Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango ( wa kwanza kushoto). Wengine ni Dr. Jehovaness Aikaeli, Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Bibi. Rukia S. Manduta, Katibu Tawala Msaidizi, Mipango na Uratibu Mkoa wa Tabora.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara amewataka maafisa mipango na wachumi kuibua miradi ya maendeleo inayotekelezeka ili kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi.

Dkt. Ntara amesema miradi mingi inayoibuliwa imekuwa haitekelezeki na siyo endelevu hivyo kuna haja ya kuzingatia mwongozo wa uwekezaji wa umma ili kuleta maendelea endelevu katika maeneo yao.
Katibu Tawala amesema hayo katika Mafunzo ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma yanayoratibiwa na Tume ya Mipango kwa Maofisa na watendaji wa Idara za Sera na Mipango wa mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Katavi.

Akizungumza katika mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Ntara amesema maafisa mipango na wachumi wanatakiwa kutoa msaada wa kitaalam kwa uongozi wa wilaya na mkoa katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Dkt. Ntara amesema mafunzo hayo yanalenga katika kuleta mabadiliko chanya katika kuibua, kutekeleza na kufuatilia miradi ya maendeleo.

Amesema fedha za miradi ya maendeleo haziwezi kupatikana kwa urahisi kama maafisa mipango na wachumi hawataandaa andiko la miradi kitaalam. “Tunaposhindwa kuibua miradi mizuri, tunashindwa kupata fedha kutoka serikalini na kwa wafadhili wengine,” alisema Dkt. Ntara.
Awali akimkaribisha Katibu Tawala, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji wa Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango, Dkt. Lorah Madete alisema Serikali  imeandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Management Operational Manual) kwa lengo la kuimarisha utendaji, uwajibikaji na kuleta ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo.
                          
Dkt. Madete amesema vipaumbele vya Serikali katika miaka mitano ijayo vimeainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambao una lenga zaidi katika kuweka mazingira rafiki ya uanzishwaji wa viwanda kwa ajili ya mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya binadamu. Kwa hiyo mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuboresha, kusimamia utekelezaji, pamoja ufuatiliaji na kufanya tathmini ya miradi ya maendeleo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa