Home » » TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ndugu, Waandishi wa Habari, Habarini za Asubuhi

Napenda kuwafahamisha kuwa nipo hapa kuwawakilisha Wanachama wenzangu wa Kikundi cha  Wakulima wa Tumbaku, kinachojulikana kwa jina la TUMAINI ITAVE ASSOCIATION cha Urambo, Mkoani Tabora chenye usajili namba S.A.19769

Kikundi hiki kinajishughulisha na kilimo cha zao la Tumbaku ambapo katika msimu wa  2014/15 kilingia makubaliano ya kuuza Tumbaku yake kupitia kwa Chama cha Ushirika cha Itundu AMCOS baada ya Kikundi chetu kushindwa kukidhi matakwa ya usajili wa Bodi ya Tumbaku ya Taifa. Katika makubaliano hayo AMCOS walikubali Kikundi chetu Kiuze Tumbaku kupitia kwenye Ushirika wao hivyo na TUMAINI ITAVE, iliomba kuuza takribani kilo 70,000 kwa Kampuni ya TLTC kwa gharama ya Dola za Kimarekani 98,770.216 ambapo malipo yake yalipaswa kufanyika kupitia Benki ya CRDB Tawi la Urambo.

Hata hivyo kabla ya malipo hayo kufanyika tuliwajulisha CRDB kuwa malipo yetu tunayapitishia katika Akaunti ya Itundu AMCO ambao ni wateja wao, Katika hali ya kusikitisha mara baada tu ya TLTC kufanya malipo , Mmoja wa Afisa katika Benki hiyo alitutaka tumpe rushwa ya Dola za Kimarekani 10, 983 ndipo akamilishe malipo yetu. Hapo ndipo ulipo ibuka mgogoro wa madai ya kuwa Fedha hizo zinazuiliwa ili kufidia deni la AMCOS walilokopeshwa na Benki ya CRDB.

Ieleweke kuwa hela tunazodai sisi TUMAINI ITAVE nizile zinazotokana na malipo halali ya Tumbaku ambayo tumeiuza kwa kupitia makubaliano na AMCOS hata CRDB Benki tuliwasilana nao wakakubali ubia huo, iweje leo waanzishe mgogoro?.

Ndugu waandishi, baada ya kutokea mgogoro huo juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuhakikisha haki yetu sisi wanyonge inapatikana.Katika kipindi hicho chote tumewasiliana na mamlaka mbalimbali ili ziweze kutusaidia kupata haki yetu.

Mnamo mwaka  2015 mwezi wa tisa tulipeleka malalamiko yetu kwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo na kufuatilia bila mrejesho, hali iliyopelekea tuchukue uamuzi wa kuwasiliana na Mbunge wa Urambo Mashariki Mhe. Margreth Sitta amaye alituunganisha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mnamo tarehe 18/12/2015. Hata hivyo kwa siku hiyo aliomba apewe nafasi ili awasiliane na watu wa CRDB ili kujua undani wa jambo lenyewe.

Kufuatia hali hiyo mnamo tarehe 21/12/2015 tulikutana na Uongozi wa CRDB Makao Makuu ambapo kikao kilifikia maamuzi ya kuundwa kwa Tume ili kuchunguza kama kweli Tumbaku imeuzwa ambapo pia Mrajisi wa Vyama Vyama vya Ushirika alishiriki kikao kile.

Pamoja na uamuzi wa kuunda tume, iliafikiwa kuwa endapo TUMAINI ITAVE itabainika imeuza Tumbaku yake kupitia Itundu AMCOS, Taarifa itapelekwa CRDB na watalazimika kuwalipa TUMAINI ITAVE huku Muhusika akiwajibishwa.

Aidha Mwenyekiti wa Itundu AMCOS, Bw. Ramadhani Matongo aliwasisitiza CRDB kulipa fedha hiyo ili kuepusha uvunjifu wa amani kwani ni makubaliano halali na hata CRDB walitaarifia na wakakubaliana nayo.

Kama tatizo ni mikopo watu waiokopeshwa wanajulikana, na bahati nzuri nyaraka zao wanazo wao kama dhamana, waendee wakakamate matrekta yao kufidia deni na siyo kuchukua fedha zisizowahusu.

Tume iliyoundwa walianza kazi rasmi tarehe 28 Wilayani Urambo ambapo walikutana na Mkuu wa Wilaya, Afisa Ushirika Mussa, Mwakilishi wa Bodi ya Tumbaku Kanda ya Magharibi, Bodi ya Itundu AMCOS, Bodi ya TUMAINI ITAVE, na wakulima Baadhi.

Baada ya tume hiyo kufanya uchunguzi wake ilibaini kuwa hakuna shaka yeyote kuwa TUMAINI ITAVE imeiuzia Tumbaku Kampuni ya TLTC T kupitia Itundu AMCOS hivyo wanastahili kulipwa hela yao.

Katika hali ya kustaajabisha taarifa iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Florence Turuka mnamo tarehe 15/01/2016 huku katika taarifa hiyo inashangaza kuona inakubali kuwa TUMAINI ITAVE wameuza Tumbaku kweli lakini hatustahiri kulipwa.
Kufuatia hatua hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Florence Turuka alimuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku kufanya uhakiki, ambapo baada ya uhakiki kufanyika ilibainika kuwa TUMAINI ITAVE iliuza Tumbaku kilo 51,741 ambayo iliuzwa kupitia Itundu AMCOS, Aidha taarifa hiyo ilibainishwa kuwa Kampuni ya TLTC ililipa JUMLA YA Dola za Kimarekani 107,795.72 kwenye  Akaunti ya Itundu AMCOS ilityopo CRDB Benki.

Fedha hizo zilizuiliwa na Benki hiyo kwa kuwa Itundi AMCOS ilikuwa inadaiwa Dola za Kimarekani 247,098.24, taarifa hiyo imebainisha kuwa kati ya fedha hizo zinazo zuiliwa Dola za Kimarekani 98,772.216 ni fedha hali za TUMAINI ITAVE zilizotokana na malipo ya Tumbaku yao.

Kufuatia taarifa hiyo ya uhakiki Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mnamo tarehe 21/04/2016 alimuandikia Mkurugenzi Mkuu wa CRDB iliyoambatana na orodha ya wakulima wanaostahili kulipwa kufuatia kuuza Tumbaku yao.

Ndugu waandishi, pamoja na jitihada zote hizo CRDB iligoma kulipa fedha hizo ndipo tukaamua chukua hatua zaidi kwa kufanya kuonana na Waziri mwenye dhamana ili atusaidie wakati huo akiwa ni Mhe. Mwigulu Nchemba mnamo tarehe 07/06/2016 katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo mjini Dodoma.

Waziri alitoa ushirikiano kwa kuwasiliana na Mkurugenzi wa CRDB ndipo Mkurugenzi alijifanya hajui suala hili wakati Waziri ameona vielelezo vyenye saini ya Kimei, ndipo akaomba apewe siku mbili kwa ajili ya kushughulikia malipo.

Katika kuendelea na juhudi za kutetea hai yetu sisi wanyonge mnamo tarehe 01/07/2016 tuliamua kumuandikia Mhe. Rais barua ili kumfahamisha namna sisi wanyonge tunavyonyanyasika, aidha tarehe 22/08/2016 niliandika tena barua kwa ajili ya kukumbushia.

Nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli aingilie katika mgogoro huu ili kutunusuru sisi maskini tulioamua kujikomboa wenyewe kwa kufanya kazi kama ambavyo yeye amekuwa akisisitiza.

Mheshimiwa Rais hali yetu ni mbaya imefikia hadi viongozi wa Kikundi wamekimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao kwani wakulima wamekuwa wakiwavamia kwa kudhania viongozi wao wamewatapeli.

Nimatumaini yetu kuwa mgogoro huu utakuwa umefikia tamati na wakulima wote wa Kikundi cha TUMAINI ITAVE watapata haki yao kwani Rais wetu ni mtetezi wa wanyonge.

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania.

Moshi Rashid Lubibi
Mwakilishi wa kutoka Kikundi cha TUMAINI ITAVE
Simu namba: +255752553839 au 0783215952



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa