Home » » BODI YA PAMBA TANZANIA YATAKIWA KUONGEZA MBEGU MKOANI TABORA

BODI YA PAMBA TANZANIA YATAKIWA KUONGEZA MBEGU MKOANI TABORA

NA TIGANYA VINCENT.
UONGOZI wa Bodi ya Pamba Tanzania umeombwa kuongeza tani 148 ya mbegu za zao hilo baada ya wakazi wengi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kwa ajili ya kulima zao hilo katika msimu wa mwa 2017/18. Ombi hilo limetolea jana katika kijiji cha Mwanasimba Wilayani Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa uzinduzi wa msimu ujao wa kilimo cha pamba nchini.

Alisema kuwa baada ya zoezi la uhamasishaji wa kufanyika katika vijiji mbalimbali kwenye Wilaya za Igunga, Uyui, Urambo, Nzega na Kaliua watu wamehamasika na kujitokeza kulima zao hilo na kusababisha upungufu wa mbegu kutoka walizokisia za awali. Mwanri alisema kuwa kabla ya zoezi hilo kulikuwa na mahitaji ya tani 672.57 lakini baada ya kuendesha zoezi hilo idadi ya wanaohitaji mbegu imeongezeka na kufikia mahitaji ya tani 820.12 wakati hadi hivi sasa wamepokea tani 672.03. Alisema kuwa Tabora ndio imechaguliwa kuwa mzalishaji wa mbegu za pamba na kitalu cha taifa  kwa ajili ya maeneo mengine nchini na kwa hiyo mbegu pekee itakayopandwa ni UKM08.

Mwanri alitoa wito kwa uongozi wa Bodi hiyo kuhakikisha kuwa upungufu wa mbegu hizo unaondolewa na zinawafikia wakulima mapema kwa sababu mvua zikishaanza kunyesha kuna baadhi ya maeneo hapa mkoani ni vigumu kufikika. Kwa upande wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Mkurugenzi wa Bodi hiyo Marco Mtunga alisema kuwa katika msimu ujao wa kilimo jumla ya tani 25,000 za mbegu zimetengwa kwa ajili ya wakulima ambapo 11,548 ni aina ya UKM08 na tani 13,452 ni UK91.

Alisema kuwa kwa upande wa Mkoa wa Tabora ikiwa ndio imechaguliwa kuwa kitalu cha taifa cha mbegu aina iliyosambazwa kwa ajili ya kulimwa katika msimu huu ni UKM08 ikiwa ni maandalizi ya mbegu kwa ajili ya maeneo mengine kwa Msimu wa 2018/19. Mkurugenzi Mkuu huyo alisisitiza kuwa baada ya hapo ni mbegu hiyo itakayolimwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Aidha Mtunga aliongeza kuwa jumla ya ekari milioni moja na laki tatu zinatarajiwa kupandwa pamba msimu ujao wa kilimo katika mikoa 16 inayolima zao hilo hapa nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo alisema kuwa tayari wameshapokea tani 500 za mbegu za pamba ambapo wameshazishambaza katika maeneo yote  yanayolima zao hilo. Alisema kuwa tayari viongozi mbalimbali wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kuzalisha kulinga na sharia na kanuni za kilimo hicho kwa ajili ya kulinda heshima ya Wilaya ya Igunga kuwa kitalu cha Taifa.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited : |
Copyright © 2012. Tabora Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa