Na Tiganya Vincent
RS-Tabora
21 Novemba 2017
WAKURUGENZI
Watendaji wameagiza kuhakikisha maeneo ya Shule na Taasisi nyingine za
elimu yanapimwa haraka na kuwekewa mipaka ili kuepuka uvamimizi
unaofanywa na watu na kusababisha migogoro ambayo imekuwa ikichelewesha
maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni mkoani Tabora na Naibu
Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais , Serikali za Mitaa na Tawala za
Mikoa( TAMISEMI ) Tixon Nzunda wakati akizungumza na Watendaji na watumishi wa Mkoa huo.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa migogoro kati ya uongozi wa Shule husika na wavamizi wa maeneo hayo.
Nzunda
alisema kuwa migogoro inayotokana na uvamizi wa maeneo ya shule imekuwa
ikiathiri maendeleo ya wanafunzi na taaluma kwa sababu uongozi wa shule
wakati mwingine umekuwa ukishindwa kupanua miundo mbinu kwa ajili ya
utoaji wa elimu kwa wanafunzi.
Alisema
kuwa ili kuepuka tatizo hilo kuendelea kujitokeza katika maeneo
mbalimbali ya shule ni kwa Wakurugenzi Watendaji kwa kushirikiana na
watendaji wengine kama vile watu wa mipango miji kuhakiki maeneo yote
yanamilikiwa na Shule na kuwaondoa ambao wameingia.
Aidha
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaagiza Wakuu wote wa Shule kuhakikisha kuwa
maeneo yao yanapandwa miti mipakani na maeneo mengine ya shule ikiwa ni
hatua ya kukabiliana na uvamizi unaofanywa na watu wanaoingia baada ya
kuona maeneo hajafanyiwa uendeleza wowote.
Aliongeza
kuwa pia wanatakiwa kupanda maeneo ya shule maua ikiwa ni sehemu ya
kufanya mazingira yavutie wanafunzi kwenda kujifunza.
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu huyo amewaagiza walimu kuhimiza pia masomo ya michezo na Sanaa mashuleni ikiwa ni sehemu ya kuwavutia wanafunzi wengi kuhudhuria shuleni.
Alisema
kuwa ni vema wakatumia fedha kidogo wanayopata kununulia vifaa vya
michezo na Sanaa ili kuwapa fursa wanafunzi kuonyesha vipaji vyao mapema
ambavyo vinaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye kama
vitaandaliwa na kulelewa vizuri toka awali.
Nzunda alisisitiza kuwa michezo na Sanaa ni sekta ambazo
zimesaidia vijana kujiari sehemu mbalimbali duniani , hivyo ni vema
walimu wasaidie kuwaandaa wanafunzi ili waweze kushiriki kikamilifu
katika eneo hilo.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora Bosco Nduguru alisema kuwa
kwa upande wao wameshaanza kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya Shule ambapo
hivi karibuni waliowaondoa wavamizi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana
ya Tabora kwa kuvunja nyumba zilizojengwa katika eneo hilo.
Alisema
kuwa wanataraji kuwaondoa wakati wowote waliovamia maeneo mengine ya
Shule kama wale wa Shule ya Sekondari MIlambo na kwingineko na kisha
kuweka uzio.
0 comments:
Post a Comment